Mfalme na Mvumbuzi

Jioni ilijivuta taratibu, kama mtu anayesita kuondoka. Kijiweni wadau wakiwa wameketi chini ya mwembe vikombe vilikuwa vimejaa nusu, huku mawazo yamejaa kupita kiasi.

Wazo Mbadala alikuwa akifinyanga kipande cha karatasi, Hekima aliwaangalia ndege wakirudi nyumbani kwa haraka, kama waepukao ghasia.

Mzee Doto alipopuliza pumzi yake ya kawaida kabla ya hadithi, sauti yake ilikuwa na uzito tofauti.

“Hapo zamani za utawala wa Mfalme Mkunjufu, katika milima ya Wagunduzi, aliishi kijana mmoja mwenye akili iliyokataa kukaa kimya. Jina lake aliitwa Tenda. Alitazama ndege akabuni, alisikiliza mito akavumbua. Kila kitu kilimfundisha.

Usiku baada ya usiku, chini ya mwanga dhaifu wa taa ya mafuta, alikunja chuma, akapima mbao, akajaribu na kushindwa, hadi siku moja akafanikiwa. Baada ya miaka ya kujikunja chini ya taa ya mafuta, alimletea Mfalme Mkunjufu kitu cha ajabu.

Halikuwa gari la farasi. Wala la ng’ombe. Lilikuwa na magurudumu mawili, mwendo mmoja, na fremu nyepesi. Mtu angekaa juu yake, akatumia nguvu za miguu yake mwenyewe, na kusafiri kwa kasi isiyofikiriwa—mara tano ya mwendo wa mtu wa kawaida. Chombo hicho hakikuhitaji maji wala chakula kuweza kutembea.

Ilikuwa ni baiskeli—ingawa jina hilo lilikuwa bado kuzaliwa.

Mfalme Mkunjufu alisimama kutoka kwenye kiti chake cha enzi. Alizunguka kifaa kile, akakigusa, akakitazama kama anavyotazama kitu kisichoeleweka.

Kisha akasema neno moja:

“Vunja.”

Tenda alipiga magoti.

“La, Mfalme! Hiki ni kifaa cha maajabu. Kitafungua njia. Watoto watafika shuleni mapema. Wakulima watafikisha mazao sokoni. Waganga watawahi kwa wagonjwa walioko mbali.”

Mfalme Mkunjufu alimwangalia kwa macho yasiyopepesa.

“Ndiyo,” alisema polepole.
“Kitaleta uhuru. Uhuru ambao haujaombwa. Uhuru usiotawaliwa.”

Akasogea karibu.

“Watu wataanza kusafiri bila idhini yangu. Wataona yaliyo nje ya mipaka yao. Watapata mawazo mapya—yasiyoandikwa katika mila zetu.”

Akasema kwa sauti ya hukumu:

“Ufalme wangu umejengwa juu ya mahali pa kila mtu: mkulima shambani, mfanyabiashara sokoni, mtawala jimboni. Kifaa chako kitavunja mahali pa kila mtu. Kitaleta watu mahali wasipostahili kuwa.”

Akatabasamu kwa huzuni fupi.

“Ustaarabu wetu utaangamia. Vunja.”

Mfalme Mkunjufu alisimama kutoka kiti chake cha enzi. Alizunguka gari hilo. Aliligusa. ‘Vunja!’ aliamua. Alimwambia Tenda.

Tenda alipiga magoti, ‘La, Mfalme! Hili ni kifaa cha maajabu! Litaleta uhuru! Watoto wataweza kufika shuleni haraka, wakulima watasafiria mazao yao kwa soko, waganga watamwokoa mgonjwa mbali!’

Mfalme Mkunjufu alimnyamazia kwa macho makali. ‘Ndiyo,’ alisema polepole. ‘Litaleta uhuru. Uhuru ambao haujaombwa. Uhuru ambao hautawaliwi. Watu wataanza kusafiri bila idhini yangu. Wataona maeneo ambayo si ya kawaida kwao. Watajifunza mambo mapya… mambo yasiyo katika kitabu cha mila zetu. Ufalme wangu unajengwa juu ya mahali pa kila mtu: mkulima shambani, mfanyi biashara sokoni, mtawala jimboni. Gari hili litavunja mahali pa kila mtu. Litachukua watu kwenye mahali wasipaswa kuwa. Ustaarabu wetu utalia. Vunja.‘”

Mzee Doto alimaliza kama alivyoanza. Kimya kikali kikateremka kijiweni. Hata kelele za mji zilionekana kusita.


Baada ya kimya cha muda mrefu, MKIMBIAJI (akionyesha baiskeli yake iliyoegeshwa kwenye mwembe):
Yaani! Huyo mfalme alikuwa mjinga kabisa. Aliogopa mabadiliko. Tenda alikuwa karibu kuiokoa nchi yake, kuirusha mbele kwa miaka mia. Huo ulikuwa upofu wa madaraka. Alikuwa amepagawa na ufalme! Aliona mabadiliko kama adui! Alipoteza fursa!”

WAZO MBADALA (akiweka karatasi chini, kwa utulivu):
Mjinga? Hebu tusimame kidogo. Ufalme wa Mkunjufu ulikuwa kama piramidi—thabiti, uliosimama kwa mfumo mmoja. Kila mtu alijua nafasi yake. Amani, chakula, usalama—vyote vilitegemea mfumo huo.

Akaongeza:

“Baiskeli ya Tenda haikuwa chuma tu. Ilikuwa wazo. Wazo kwamba mtu anaweza kuvuka daraja la nafasi yake. Kwamba umbali—ngome kuu ya mamlaka ya mfalme—ungeweza kushindwa na miguu miwili tu.”

Mfalme hakuona ujinga. Aliona mwisho wa ulimwengu alioujua.

“Alichagua utulivu wa kizamani badala ya ghasia ya maendeleo. Swali ni moja: kiongozi afanye nini—awalinde watu dhidi ya hatari ya mabadiliko, au awaingize kwenye giza la kesho lisilojulikana?”

Minong’ono ikaanza:
“Ana hoja…”
“Lakini maendeleo hayaepukiki!” “Yeye alikuwa mnyanyasaji!”

Hekima alichukua kikombe chake cha kahawa na kuweka kando na kuongeza maji kwenye birika na kuchochea jiko la mkaa huku akiangalia moshi mwembamba unavyopaa.

Hekima: “Ninasikia hoja zote. Wazo Mbadala, unaona mpango wa mfalme. Lakini swali langu ni hili: Kwa nini kuvunja? Kwa nini kukataa kabisa? Je, Mfalme Mkunjufu hangeweza kuwa mwerevu zaidi? Hangeweza kumwambia Tenda, ‘Kifaa chako ni chenye akili. Lakini hakina nafasi katika ufalme wangu kwa sasa. Tunachukua. Tutakiweka kwenye ghala la vito, tutakifanyia uchunguzi na askari wetu. Labda siku moja kitatufaa…’ Kwa kufanya hivyo, angeuua wazo bila kumwua mvumbuzi. Au angeweza kumtenga Tenda, kumfanya kuwa fundi wa serikali pekee, akitumia ubunifu wake kwa ajili ya jeshi la mfalme. Hata kuvunja, kulikuwa na njia nyingine: kufanya ibada, kuliteketeza mbele ya umma kama dhabihu kwa miungu. Alichagua kitendo cha nguvu zaidi na cha kukandamiza zaidi.

Akatikisa kichwa.

“Alichagua njia ya nguvu zaidi, ya kukandamiza zaidi. Je, hiyo ilikuwa hekima ya hofu, ujanja wa kukaa kwenye madaraka au upungufu fikra?

Kijiwe kiligeuka na majadiliano makali. Je, Mfalme alikuwa mlindaji wa utamaduni au bwana mtawala mwovu? Je, Tenda alikuwa kijana jasiri au mhariri wa amani? Je, kuvunja kifaa kulikuwa uhalifu dhidi ya mustakabali, au jambo la lazima la kudumisha usawa?

Mzee Doto alisimama, na kujinyoosha. Hakuwa amesema neno moja tangu mjadala uanze. Alitabasamu kwa kina na akaingia ndani ya usiku mweusi wa mji, akiwa ameacha chungu cha mawazo nyuma yake.

Nilijikuta naangalia gari la baiskeli la Mkimbiaji. Kifaa rahisi kilichobadilisha ulimwengu. Je, kama kungekuwa na wafalme Wakunjufu duniani pote na wote wangeshinda leo tungesafirije? Je, ni haki ya kiongozi kuzuia uvumbuzi kwa ajili ya amani? Na je, mvumbuzi ana wajibu gani kwa jamii yake? Je, kuvumbua kitu kisichostahili wakati wake ni hekima au wazimu?

Jioni hiyo, nilikifunza kuwa wakati mwingine, gari si gari tu. Ni wazo. Na wakati mwingine, maamuzi ya mfalme si ukatili pekee bali ni hofu. Na kati ya wazo na hofu, ndio mahali hekima ya kweli inapaswa kutawala.

Hadithi ya Mfalme na Mvumbuzi ilikoma, lakini swali la Hekima liliishi: Kwa nini kuvunja, wakati unaweza kufunza?

Episode 3 of 7