Kama kawaida yake mzee Dotto alivyowasili kijiweni na kuketi moja kwa moja alianza simulizi yake, akielewa fika katika kijiwe hiki simulizi zake ndio kitafunio cha kusukumizia kahawa…
Katika kijiji cha Milele, palipopewa jina kwa matumaini kuliko hali, aliishi mkulima mmoja aliyekuwa na bidii kama sisimizi asiyepumzika. Jina lake aliitwa Chanda. Shamba lake halikuwa shamba la rutuba, bali lilikuwa uso wa dunia uliopasuka kwa kiu—udongo wa manjano na kijivu, mgumu kama moyo wa ukame. Kila mwaka alipanda kwa machozi, alipalilia kwa subira, na alisubiri kwa imani. Lakini mavuno yalirudi yakiwa machache, yamechoka kama tumbo lake.
Mwaka mmoja, ukame haukuja kwa adabu. Ulivamia. Mito ikajisalimisha, mawingu yakapita bila kusalimia, na nyasi zikageuka kuni. Watoto wa Chanda walilia njaa, ng’ombe wakawa mifupa inayotembea, na matumaini yakaanza kufa taratibu, kama jani la mwisho shambani.
Siku moja, baada ya sala nyingi zisizo na majibu, Chanda alijikunyata kwenye mabaki ya shamba lake. Aliinua macho yake yaliyokuwa mazito kwa uchovu na hasira, akatazama anga lililokuwa la rangi ya majivu.
“MUNGU!” alipaza sauti. “Unanisikia? Unaniona? Nimekuchumia kwa mikono hii! Nimepanda, nimevumilia! Sasa—nipe haki yangu. NINIA MVUA!”
Anga likabaki kimya. Kimya kilichochoma kuliko jua.
Kisha, sauti ikaja. Haikuwa ya radi, wala ya upepo. Ilikuwa nzito kama mlima, lakini laini kama usiku wa pwani:
“Nimekupa.”
Chanda alishtuka. “Umenipa nini, nami sina chochote?”
Sauti ikasema tena:
“Nimekupa mangoki (jembe zito la kuchimbia udongo mgumu). Yanaweza kupenya udongo. Yanaweza kuchimba. Kwenye mlima wa pembezoni mwa kijiji chako, kuna chemchem iliyofichwa. Nimekuonyesha mahali pake. Sasa, chukua nguvu zako, chimba mfereji, ulete maji shambani mwako. Mvua ni yangu. Jitihada ni yako.”
Mzee Doto alipumua kwa kina, akainua kikombe chake cha kahawa kana kwamba anakitazama kimpatie mtiririko wa simulizi
“Chanda alisimama hapo muda mrefu,” “Aliyatazama mangoki yake—vyombo vilivyomuumiza na kumwokoa maisha yake kwa miaka. Aliwaona watoto wake, mifupa yao ikisukumana chini ya ngozi. Akautazama mlima ule wa mbali. Halafu akatazama tena anga, lilelile lililokaa kimya.”
“Hakubishana tena. Alichukua jembe, akachukua mangoki, akawaambia watoto wake: ‘Kuna chemchem kule tutaileta hapa.’”
Mzee Doto akanyamaza. Hadithi ikasimama. Kijiwe kikavuta pumzi.
Kimya kilipasuliwa na sauti ya Mama Nia, mkulima aliyekuja mjini lakini bado na vumbi la mashamba moyoni.
“Huyo Mungu! Ati mwenye huruma? Anamwambia mtu mwenye njaa, mwenye watoto wanalia, aende akachimbe tena? Kama alijua chemchem iko wapi, kwa nini asitume mvua hata matone machache? Au amletee malaika wachimbe? Hii si huruma—hii ni mateso! Chanda alipaswa kutupa jembe angani na kusema, ‘Nimechoka, fanya kazi yako!’”
Maneno yakaanza kuchipuka kijiweni: “Ni kweli!” — “Lakini huwezi kumtupia Mungu lawama!”
Wazo Mbadala akasogeza karatasi yake. Juu yake aliandika neno moja: KUPOKEA. Chini yake akaongeza jingine: USHIRIKIANO.
“Mama Nia, (alianza Wazo Mbadala)…, unaona kutelekezwa. Lakini hebu tuangalie kwa jicho jingine. Mungu hakumwambia Chanda, ‘Kaa, nitakuletea chakula.’ Wala hakumwambia, ‘Kufa.’ Alimwambia, ‘Nimekupa.’ Alimkumbusha uwezo aliouona kuwa mdogo: mikono yake, akili yake, na vyombo vyake.
Chemchem haikuwa hadithi—ilikuwa halisi. Kwa mara ya kwanza, Chanda hakuwa ombaomba. Alikuwa mshirika. Kabla ya hapo, alikuwa anamwomba Mungu afanye kazi yake. Baada ya hapo, alipewa heshima ya kufanya kazi pamoja na Mungu. Je, hiyo ni adhabu… au ni heshima ya juu kabisa?”
Hekima alikuwa amekaa kimya, akitazama chungu cha maji moto. Alimimina maji baridi. birika likafoka, likipiga kelele, kama vile likilalamika kwa kucheleshwa kuwekewa kimininika.
“Ninaona ushirikiano. Lakini swali langu ni hili: Kwa nini kuficha chemchem? Kwa nini kuisubiri hadi watoto walie njaa? Kama Mungu alijua mwisho, alijua pia mwanzo. Angeweza kusema mwaka mmoja kabla: ‘Chanda, chimba sasa.’
Ahadi ilikuwapo, ndiyo. Lakini wakati wa kuitoa—je, ilikuwa ni hekima, au ni mwenye nguvu anayepima imani kwa maumivu?”
Kijiwe kikawa kizito. Hakuna aliyekuwa na jibu rahisi.
Hekima akaendelea, lakini unaweza ukasema pia kwanini Chanda alisubiri mpaka ukame uwasili na asijitayarishe na uwezekano wa ukame ? Unaweza kusema alitumia mbinu zote alizoweza, lakini kama Chemchem kweli ipo nyuma ya mlima huenda kilichotokea leo ni funzo kwa ajili ya kesho, shida za leo zimemuwezesha kupata ahueni ya keshokutwa…., Bila Ukame asingegundua uwepo wa Chemchem
Ugumu wa Maisha ni Kipimo cha Akili – Alidakia Muhenga
Mzee Doto alisimama polepole, macho yake akiyapeleka kila kona, kama kurunzi ifukazayo giza.
“Chanda alichimba,” alisema. “Hakumaliza mfereji. Alitumia nguvu yake ya mwisho. Alifariki karibu na chemchem, mikono yake imevimba, damu ikiwa imechanganyika na udongo. Ndugu zake waliendeleza kazi. Maji yalifika kijijini siku ya mazishi yake.
Leo, kijiji kinaitwa Chemchem ya Chanda.”
Onaona sasa ? Kifo cha Chanda kingeweza kuepukika iwapo Chemchem hio ingegunduliwa kabla ya…..
Sasa igunduliwe vipi wakati kabla wakati kulikuwa hakuna uhitaji kama sasa ? Alisema Shehe mmoja aliyekuwa kimya kwa muda mrefu na hakupendezwa na imani finyu ya mama Nia…, Bila watu kuwa na Imani kwamba kilichosemwa kwamba kweli kipo (Chemchem) wangekata tamaa na wasingechimba na huenda badala ya Chanda pekee kijiji kizima kingekumbwa na mauti…
Nilikaa nikitazama vikombe vilivyojaa na vingine vikiwa nusu. Je, Chanda alikufa kwa utii? Kwa ukaidi? au Kwa imani? Je, Mungu alimjibu ombi lake—au alimpa jibu tofauti, jibu lililomwangusha lakini likainua kizazi chake?
Je, majibu ya maisha yako milimani mwetu, yakisubiri kuchimbwa kwa maumivu? Au hekima ni kujua ni wakati gani wa kuomba mvua, na wakati gani wa kushika jembe?
Watu walianza kuondoka mmoja mmoja, mimi nikiwa katika lindi la mawazo nikasikia sauti ya Muhenga kama vile anaongea peke yake na sio kwa ajili ya umati
Episode 4 of 7“Aliyepewa jembe, asiilalamikie ardhi kabla hajachimba.”

