Ahadi ya Miujiza

Kama ilivyokuwa desturi yake, baada ya kufika kijiweni Mzee Doto alikaa kimya kwa muda, akitazama vikombe vya kahawa kana kwamba vilikuwa vinaficha majibu ya maswali ya dunia. Alipoketi vizuri, alianza na simulizi zake, Zamani za kale, wakati ardhi ilipokuwa inalia damu na hewa ikijaa wito wa uhuru, kulikuwa na mzee mmoja katika kijiji kilichoitwa Mashujaa. Jina lake lilikuwa Mbeba Maono.

Siku moja, kikosi cha wakoloni kilikaribia kijijini—bunduki zao zikiwa kali kama meno ya chui, nyoyo zao zimejaa kiburi na hasira. Kila mtu alijua dhamana ya wakoloni, nchi ilipoangukia kwenye utawala wao ilikuwa kama mtoto aliyefungwa mikono na miguu. Watu walichapwa, walitozwa kodi, walibebshwa mizigo pasipo kuelewa sababu.

Wakulima, wavuvi, wakina mama na watoto… wote walijikusanya kwenye uwanja. Hofu ilitawala. ‘Tutafanya nini?’ wakapiga kelele. Mbeba Maono alisimama mbele yao. Miaka ilikuwa imemlalia mabegani kama mzigo mzito, lakini macho yake yalikuwa hai, yakimetameta kama moto wa mbali. Hakuwa na upanga. Hakuwa na bunduki. Aliinua mkono wake uliojaa mishipa, akasema kwa sauti iliyovunjika lakini nzito kama ngurumo:

“Watoto wangu! Msihofu! Leo, bunduki za adui zitatumia maji, si risasi. Kila risasi itageuka chemchemi! Mungu wa babu zetu ameyaona mateso yenu!”

Kauli hiyo, kama mwanga uliofunuliwa kwenye giza, ilibadilisha hofu kuwa shauku. Maneno yale yakashuka kama mvua juu ya ardhi kavu. Hofu ikageuka shauku. Unyonge ukageuka ujasiri.

Kijiji kikazima kwa kelele za vita.

Kwa visu, mikuki, mawe—na imani.

Damu ilimwagika, ndiyo. Watu walianguka. Lakini siku ile, kijiji cha Mashujaa hakikuanguka mikononi mwa mkoloni. Wachache waliishi na kuendelea kupigana.

(Mzee Doto ananyamaza na kuelekeza mawazo yake kwenye kikombe chake cha kahawa kama vile anahesabu matone yaliyobaki. anakaa kimya, akiacha maneno yake yazame kwenye akili za wasikilizaji, kama mvua inyesheayo ardhi kavu.

Kimya. Kisha… mlolongo unavunjika.

Juma (mkulima): “Lakini… hiyo imani ilikuwa potofu! Risasi hazikugeuka maji! Watu walifariki! Je, mzee yule hakuwa mjinga? Aliwapeleka watu wake kwenye mauti kwa uwongo!”

Hapo ndipo Wazo Mbadala anaposugua mawani yake na kusema.

Mjinga? Ngoja tuangalie kwa makini. Kwa nini watu wa Mashujaa walisimama siku ile? Si kwa sababu walijua mbinu za vita, bali kwa sababu waliamini na hofu haikuwa tena kikwazo kwao.

“Mbeba Maono aliwapa watu kitu kilichozidi nguvu ya bunduki—ushujaa. Bila kauli ile, wasingeweza hata kuinua fimbo.”

Je, alikuwa nabii wa uwongo? Au kiongozi aliyelazimika kutumia uwongo mkubwa kupambana na adui mkubwa zaidi ambaye ni hofu na unyonge?

Mjadala unawaka. “Ana ukweli!” “Lakini ni hatari!” “Ingefanyika vipi kama…”

Ndipo Hekima anaposonga mbele kidogo, kikombe chake cha kahawa kwenye mikono yake.

Hekima: “Ninasikia mjadala. Wazo Mbadala, unaelewa hisia. Lakini swali langu ni hili: Je, hakukuwa na njia nyingine? Badala ya kuwaahidi maji yasiyowekea akilini, angewezaje kusema, ‘Risasi ni hatari, lakini pia ni chache. Tutajificha kwenye mashamba, tutawavamia kutoka pande zote, tutatumia giza kama silaha?’ Hiyo ingewaongoza, isiowapelekea kwenye mlango wa risasi moja kwa moja. Imani ni nzuri. Lakini hekima ya kupanga, je, si bora zaidi?”

Wazo Mbadala anajibu, “kumbuka hapa adui mkubwa zaidi ni uoga na kuogopa kitu chenye nguvu zaidi, sasa watu wakishaamini kwamba mishale yao ni hafifu kwa risasi hata useme nini hawatakuelewa… hatua kwa hatua, kwanza unamalizana na adui wa kwanza ambaye ni hofu. Mtu aliyepoozwa na hofu hasikii ramani wala mkakati. Lazima kwanza umtoe gizani, hata kwa uwongo.

Lakini kwenda kama kipofu kwenye nyumba ya moto inayoteketea wala sio ujanja bali ni….

Mbadala anamkatiza unasema kwenda kwenye nyumba ya moto kama vile unapotoka napo hakuna moto, hapa uhalisia ni kwamba nje panawaka na ndani panawaka ingawa ndani kuna uwezekano wa kupata vifaa vya kuzimia moto…., sasa chaguo ni la kufa nje bila kujaribu au kuingia ndani na kubahatisha kuzima moto

Hekima anadakia, ni kweli usemayo, hatuwezi kusema kipi kilikuwa sahihi kwa wakati husika bila ya sisi kuwepo na kujua kulikuwa na njia ngapi tufauti na huenda hii ndio ilikuwa njia ya mwisho. Lakini badala ya kusema zinageuka maji labda angesema unapewa idadi kadhaa ya risasi kukuona, ikipigwa ya kwanza mpaka ya tatu zinakuwa maji zikipigwa nyingi zinakuwa risasi, hivyo hii ingepelekea watu kujificha na kutumia umakini kidogo kuliko kwenda moja kwa moja, ukizingatia uongo hufanya kazi mpaka pale unapogundulika sio ukweli, unadhani baada ya watu kuona wenzao wanaanguka kama nzige si hofu ingewarudia maradufu ? Ukizingatia huenda wakoloni walikuwa wachache na bunduki chache na kila bunduki ilikuwa na risasi moja hivyo kuchukua muda kujaza nyingine hapo kama kuna watu kumi utamuangusha mmoja na wengine tisa watamaliza kazi…

(Muhenga, aliyekuwa kimya muda wote, anainua macho taratibu.)

MUHENGA:
Aliyeogopa kufa, hawi tayari kuishi. Lakini asiyejua pa kusimama, hata akiishi, hupotea.

(Ananyamaza tena.)

Kijiwe kinageuka kuwa duara la mawazo. Kila mtu ana maoni. Mzee Doto anaangalia kwa macho yaliyofifia, akitabasamu kidogo. Hakukuwa na jibu moja. Lengo lake lilikutana.

Na hivyo, jioni hiyo ilikwenda. Kahawa ikapungua, lakini mawazo yalizidi kuongezeka. Maji yaliyogeuka risasi? Au imani iliyogeuka ushujaa? Uongo uliotoa ukweli? Swali la Hekima lilizama kwenye kichwa changu: Njia gani ya uongozi ni bora: kuwatia nguvu rohoni kwa ahadi ya miujiza, au kuwapa mkakati wa kukabiliana na hatari kwa uwazi?

Hadithi ya Mbeba Maono ilikoma, lakini mchezo wa mawazo… ndio kwanza ulianza.

Episode 2 of 7