Dhahabu ya Machozi

I

Jua la asubuhi lilimwaga mwanga wake wa dhahabu juu ya nyuso za wanaume sita waliosimama kando ya shimo. Lilikuwa la kwanza kati ya dhahabu mbili – ile ya anga na ile ya ardhi. Shija alikwisha pumzika kwa dakika tano tu, kofia yake ya iliyotengenezwa kwa kutumia shati lake lilichanika chanika ikiwa imeshaiva jasho la asubuhi.

“Twende, wanaume,” alisema Bwana Rajabu, msimamizi wa eneo hilo la uchimbaji. “Hiyo dhahabu haijichimbi yenyewe.”

Shija alishuka tena kwenye shimo lenye kina cha mita kumi na mbili. Ardhi ilikuwa imejaa mawe makali na udongo mgumu. Kila chepe alilolipiga lilikuwa na maombi mawili: la kwanza, kupata kidonge cha dhahabu. La pili, kuokoka hai. Mara nyingine upigaji wa chepe unaweza kusababisha mwisho wa uhai kwa shimo kuwafunika wote waliomo ndani.


II

Miaka mitatu iliyopita, Shija alikuwa mkulima mdogo wa mahindi na mhogo. Shamba la babake lilikuwa na ukubwa wa hekta mbili tu. Kila msimu, mavuno yalikuwa yakipungua. Wazee walisema ni kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi. Daktari wa wilayani alisema ni kwa sababu ya kemikali zilizotumika miaka iliyopita.

Siku moja, jamaa yake Mussa alimtembelea. Mussa alikuwa na gari jipya – Toyota ist ya rangi ya dhahabu.

“Unafanya kazi gani sasa?” Shija alimuuliza, macho yake yakiwa yamejaa mwanga wa gari hilo.

“Ninachimba,” Mussa alijibu kwa fahari. “Dhahabu, ndugu. Dhahabu ya Machimboni.”

Mussa alimwelezea kuhusu pesa anazozipata. “Kwa siku moja nzuri, unaweza kupata zaidi ya unayopata kwa mwezi mzima kwenye shamba.”

Siku tisa baadaye, Shija alikuwa ameshaacha jembe na kuchukua suluhu na koleo.


III

Saa saba za mchana, Shija alipata. Kidogo tu – gramu mbili ya dhahabu safi. Alitoa ukelele mfupi wa furaha. Wenzake wakakurupuka.

“Hongera, mzee!” walimkaribisha.

Bwana Rajabu alikuja na mizani yake ndogo. “Gramu mbili kamili,” alisema. “Haya, hii ni yako.” Akampa Shija noti ya shilingi elfu kumi.

Shija alizingatia mkononi mwake. Dhahabu aliyoichimba ilikuwa na thamani ya zaidi ya shilingi laki tano. Yeye alipata elfu kumi tu.

“Kwa nini?” alimuuliza Bwana Rajabu.

“Usiulize maswali, Shija. Unajua sheria. Mimi nanunua, wewe unauza. Chakula nachokupa kila siku, vifaa navyoleta hapa na kumbuka haya mashimo ni yangu, unadhani hizo gharama zote analipa nani ? Huo ndiyo mkataba”

Mkataba ambao hakuwahi kuusaini. Mkataba ambao ulikuwa umeandikwa kwa lugha ya nguvu na ufukara.


IV

Jioni, baada ya kazi, Shija alifika kwenye banda lake dogo. Alikuwa na chombo kidogo cha plastiki kilichojaa kemikali nyeupe – zebaki. Alimimina juu ya mchanga aliochukua kutoka shimoni, akachanganya kwa mkono wake.

Zebaki ilikusanya vipande vidogo vya dhahabu vilivyokuwa vimejificha kwenye mchanga. Alikuwa akifanya hivi kila siku kwa miaka mitatu. Kila siku, zebaki hiyo hiyo ilipita kwenye ngozi yake, kupenya damuni, na kujenga maskani katika kifua chake.

Mara nyingi alikuwa akikohoa usiku. Mara nyingi alijisikia kizunguzungu. Lakini elfu kumi kwa siku zilikuwa dawa ya maumivu yote.


V

Siku ya Jumatatu, Shija alimwona mgeni. Mzungu mwenye umri wa miaka thelathini, aliyevaa suruali fupi na T-shirt. Alikuwa na mizani sahihi na vifaa vya kisasa.

“Habari,” mgeni alisema kwa Kiswahili chenya lafudhi ya kigeni. “Mimi ni David. Ninatoka Uingereza. Ninafanya utafiti.”

David alimuuliza Shija maswali mengi: Unachimba siku ngapi kwa wiki? Unapata kiasi gani? Unatumia kemikali gani?

Mwishowe, David alimwonyesha kwenye simu yake ya mkononi. “Unajua hii dhahabu unayochimba, inaenda wapi?”

Alionyesha picha ya duka la vito huko Ughaibuni. “Hapa ndio inauzwa. Peti hii moja,” alionyesha peti ya dhahabu safi, “ina thamani ya pauni elfu mbili. Hiyo ni sawa na shilingi milioni saba.”

Shija alihesabu kichwani: Gramu tano kwa siku, siku ishirini kwa mwezi, miezi kumi na mbili kwa mwaka… miaka mitatu…

Alipata jibu: Kwa miaka mitatu alikuwa amechimba dhahabu yenye thamani ya takribani shilingi bilioni moja.

Na yeye mwenyewe alipata shilingi milioni kumi na nane tu.


VI

Mwezi uliofuata, Shija alianza kuhisi maumivu makali upande wa kulia wa tumbo lake. Alikwenda kwa daktari wa wilayani.

“Una hitaji kufanya CT scan,” daktari alisema baada ya kumkagua. “Lakini hatuna hapa. Lazima uende mkoani.”

Shija alitumia akiba yake yote – shilingi milioni moja – kwa safari na matibabu ya mjini.

“Tunahitaji kuanza kemotherapy,” daktari alisema. “Gharama ya kizazi kimoja ni shilingi milioni mitatu. Tunahitaji vizazi sita.”

Shija alianza kuhesabu tena: Milioni tatu mara sita… milioni kumi na nane…

Alikaa kwenye kiti cha hospitalini, karatasi ya matokeo mkononi mwake. Alikumbuka hesabu ya David: Bilioni moja ya dhahabu nimeichimba… milioni kumi na name nimepata… sasa nataka milioni kumi na nane kwa matibabu…


VII

Siku mbili baadaye, Shija alirudi machimboni. Hakwenda kwenye shimo. Badala yake, aliketi chini ya mti mkubwa wa mbao, akitazama eneo la uchimbaji.

Aliwaona wanaume wengine wakishuka kwenye shimo, kama mchwa wakishusha malimbo yao ya mifupa. Aliwaona wakitoa mchanga, wakipumzika kidogo, wakishuka tena.

Alimwona Bwana Rajabu akiwa na mizani yake, akiwaangalia kwa macho makali.

Aliona lori kubwa ikija kuchukua mchanga uliochambuliwa, kwenda kwenye kiwanda cha kusafisha dhahabu.

Akakumbuka David na duka la vito huko ughaibuni. Akakumbuka peti ya shilingi milioni saba.

Machozi yalianza kutoka machoni mwake. Sio machozi ya uchungu au huzuni. Bali ya ufahamu.


VIII

Usiku huo, Shija aliandika katika daftari lake:

Mimi nimechimba dhahabu yenye thamani ya bilioni moja ya shilingi.
Nimepata milioni kumi na nane.
Bwana Rajabu amepata mia moja ya milioni.
Wauzaji ughaibuni wamepata mabilioni.
Na sasa, ninaugua kwa sababu ya dhahabu hiyo.
Matibabu yanagharimu milioni kumi na nane – pesa zangu zote.
Mto wetu umepoteza samaki wote, kwa uchafuzi wa mazingira.
Watoto wetu wanakohoa usiku.
Nani mnufaika?

Na nani anateswa?

Episode 1 of 10